Proverbs 10

Mithali Za Solomoni

1 aMithali za Solomoni:

Mwana mwenye hekima
huleta furaha kwa baba yake,
lakini mwana mpumbavu
huleta huzuni kwa mama yake.

2 bHazina zilizopatikana kwa njia mbaya hazifai,
lakini uadilifu huokoa kutoka mautini.

3 c Bwana hawaachi waadilifu kukaa njaa,
lakini hupinga tamaa ya mtu mwovu.

4 dMikono mivivu hufanya mtu kuwa maskini
lakini mikono yenye bidii huleta utajiri.

5 eYeye akusanyaye mazao wakati wa kiangazi
ni mwana mwenye hekima,
lakini yeye alalaye wakati wa mavuno
ni mwana mwenye kuaibisha.

6 fBaraka huwa taji kichwani mwa mwenye haki,
lakini jeuri hufunika kinywa cha mwovu.

7 gKumbukumbu ya mwenye haki itakuwa baraka,
lakini jina la mwovu litaoza.

8 hMwenye hekima moyoni hupokea maagizo,
lakini mpumbavu apayukaye huangamia.

9 iMtu mwadilifu hutembea salama,
lakini mtu aendaye katika njia zilizopotoka atagunduliwa.

10 jYeye akonyezaye kwa nia mbaya husababisha huzuni,
naye mpumbavu apayukaye huangamia.

11 kKinywa cha mwenye haki ni chemchemi ya uzima,
lakini jeuri hufunika kinywa cha mwovu.

12 lChuki huchochea faraka,
lakini upendo husitiri mabaya yote.

13 mHekima hupatikana katika midomo ya wenye kupambanua,
lakini fimbo ni kwa ajili ya mgongo wake asiye na ufahamu.

14 nWenye hekima huhifadhi maarifa,
bali kinywa cha mpumbavu hualika maangamizi.

15 oMali ya tajiri ni mji wake wenye ngome,
bali ufukara ni maangamizi ya maskini.

16 pUjira wa wenye haki huwaletea uzima,
lakini mapato ya waovu huwaletea adhabu.

17 qAnayekubali kuadibishwa yuko katika njia ya uzima,
lakini yeyote anayepuuza maonyo hupotosha wengine.

18 rYeye afichaye chuki yake ana midomo ya uongo,
na yeyote anayeeneza uchonganishi ni mpumbavu.

19 sWakati maneno ni mengi, dhambi haikosekani,
lakini yeye ambaye huzuia ulimi wake ni mwenye busara.

20Ulimi wa mwenye haki ni fedha iliyo bora,
bali moyo wa mwovu una thamani ndogo.

21 tMidomo ya mwenye haki hulisha wengi,
lakini wapumbavu hufa kwa kukosa ufahamu.

22 uBaraka ya Bwana hutajirisha,
wala haichanganyi huzuni.

23 vMpumbavu hufurahia tabia mbaya,
lakini mtu mwenye ufahamu hupendezwa na hekima.

24 wKile anachoogopa mwovu ndicho kitakachompata;
kile anachoonea shauku mwenye haki atapewa.

25 xTufani inapopita, waovu hutoweka,
lakini wenye haki husimama imara milele.

26 yKama siki ilivyo kwa meno na moshi kwa macho,
ndivyo alivyo mvivu kwa wale waliomtuma.

27 zKumcha Bwana huongeza urefu wa maisha,
lakini miaka ya mwovu inafupishwa.

28 aaTarajio la mwenye haki ni furaha,
bali matumaini ya mwovu huwa si kitu.

29 abNjia ya Bwana ni kimbilio kwa wenye haki,
lakini ni maangamizi ya wale watendao mabaya.

30 acKamwe wenye haki hawataondolewa,
bali waovu hawatasalia katika nchi.

31 adKinywa cha mwenye haki hutoa hekima,
bali ulimi wa upotovu utakatwa.

32 aeMidomo ya wenye haki inajua kile kinachofaa,
bali kinywa cha mwovu hujua kile kilichopotoka tu.
Copyright information for SwhNEN